Tuesday, July 18, 2017

Karibu katika sehemu ya kwanza ya simulizi tamu ya maisha iitwayo 'SITOISAHAU FACEBOOK'

                                                  RIWAYA: SITOISAHAU FACEBOOK.
                                                         MTUNZI: Emmy John P​




                                                       SEHEMU YA KWANZA

"Isabela….Isabela…" nilisikia sauti ya mwanamke ikiniita, niligeuka mara moja maana sauti ile ni kama niliwahi kuisikia mahali. Lakini sikukumbuka ni wapi. Giza totoro lilinizuia kuweza kumtambua mtu yule aliyeniita kwa ufasaha kiasi kile tena gizani.
Nilianza kujiuliza iwapo nirejee nyuma kurudi kumtafuta ama niendelee mbele ambako pia sikuwa na uhakika ni wapi. Manyunyu ya mvua yalikuwa yamenilowanisha hasa na nguo yangu ilikuwa imeshikana na mwili. Nilikuwa natetemeka huku michubuko kadhaa katika mwili wangu ikiniwashawasha. Kilikuwa kitendawili aidha niende mbele ama nirudi nyuma kuifatiliza hiyo sauti.
Ile hali ya kujiuliza niende mbele ama nirudi nyuma ikanifanya niwe kama naigiza igizo lisilokuwa rasmi.

"Isabelaaaa!!!." Iliita tena sauti hii. Sasa ilisikika dhahiri kuwa sauti ile ilikuwa katika kulia, mwenye sauti ile alikuwa katika uchungu mkubwa na bila shaka aliuhitaji sana msaada wangu. Nilitamani kuitika lakini midomo ikawa mizito. Nilipolazimisha kuitika nikawa kama nanong'oneza, sauti haikutoka. Koo lilikuwa limekauka sana. Hapo ndipo nikagundua kuwa nilikuwa na kiu sana.
Nikiwa bado katika kigugumizi mara nikasikia kama hatua za mtu ama mnyama zikikatiza taratibu. Mara moja nikajiziba mdomo wangu, pumzi zangu zisiweze kusikika kwa huyo mtu. Sikuamini hata kidogo kwamba huyo anaweza kuwa yule mwanadada aliyekuwa ananiita kwa jina langu, maana huyo alisikika kutokea upande mwingine na wala sio huu aliosikika huyu anayekatiza. Nikaamua kutulizana.

Baada ya muda pakawa kimya, kwa tahadhari kubwa nikaanza kunyata kwa kutembelea vidole kwa mbele vya miguu. Moyo ulikuwa katika mwendo kasi ambao hapo kabla sikuwahi kuufikiria.
Moyo wangu ulikuwa katika majuto makubwa na tamaa yangu ilikuwa inaniponza sasa. Pesa nisizozitolea jasho zikawa zimenifikisha katika maluweluwe haya. Maluweluwe ya kutisha. Ulimwengu ukawa unanihukumu.
Nilimfikiria yule dada aliyekuwa ananiita, nilielewa kabisa kuwa nilikuwa namfahamu lakini swali likaja.
Anaitwa nani?? Ni wapi tulionana??
Baada ya dakika thelathini za kutangatanga katika kipori hicho kidogo hatimaye niliifikia barabara.
Ilikuwa ni barabara ya vumbi ukubwa wake ulikuwa unatosha gari kupita bila wasiwasi. Nikaamua kuifata barabara ile ili niweze kutoka eneo lile la hatari kabisa. Niliifata barabara ile kwa urefu mkubwa sana…miguu ilichoka lakini sikuwa tayari kukubali kukaa chini. Hata kama ningelia kwa wakati ule isingesaidia kitu nilikuwa katika hali ngumu sana.

MIEZI SITA NYUMA

Maisha ya chuo yalikuwa yamenipiga haswa, mwalimu Nchimbi ambaye ni mama yangu mzazi naye alikuwa ameungana na waalimu wenzake katika mgomo wa nchi nzima dhidi ya masilahi finyu ya waalimu hivyo hakuwa na senti yoyote ya kuweza kunisaidia, baba naye alizidi kupata umaarufu katika vilabu vya pombe kwa kucheza na kuimba hovyo baada ya kuwa amegida za kutosha.
Kaka yangu alizidi kuchanganywa na madawa ya kulevya huku dada yangu mkubwa akiwa bize na ulokole aliouamini kuliko hata mume wake waliyezaa naye watoto watatu. Sikuwa na mtu yeyote wa kumwomba msaada kwani kaka yangu mwingine ambaye kidogo alikuwa anajiweza alikuwa haambiliki wala hashikiki mbele ya mke wake halafu kibaya zaidi mke wake tayari tulikuwa tumegombana.
Mkopo wa asilimia ishirini niliokuwa napokea ulikuwa unaishia katika kulipa madeni.

Maisha yalikuwa yameniwia magumu sana, na marafiki hawakuwa na kikubwa cha kunisaidia.
Muda wangu mwingi nilikuwa naupoteza katika kusoma vitabu na pia kuperuzi mitandao ya kijamii, facebook ukiwa namba moja. Picha zangu ziliwafanya watu wengi wasiweze kuamini kuwa nina matatizo lakini ukweli nilikuwa naujua mimi binafsi.
Kawaida ya wavulana walikuwa hawaishi kutoa maombi yao ya kuwa wananipenda lakini nilijaribu kuwakwepa kwani niliamini kuwa kujiingiza katika mahusiano ni sawasawa na kujiongezea matatizo katika maisha yangu kwani wanaume hawaaminiki hata kidogo.
Kila mwanaume huwa ana mbinu zake za kumuingia msichana, na mimi kama msichana nilikuwa nimezikariri na kumwelewa mwanaume iwapo anakaribia kunitongoza ama la. Lakini kati ya wanaume wote aliibuka mwanaume mwingine naweza kumuita wa ajabu kupita wote. Yeye alikuwa hatabiriki leo mara anaelekea kwenye mapenzi mara kesho siasa, akisema leo kuhusu mpira wa miguu basi siku nyingine ataleta masuala ya dini.

Jina lake lilisomeka kwa kifupi kama Dk. Davis. Na kamwe sikuwahi kulijua jina lake kamili zaidi ya kujua kuwa anaitwa dokta davis. Kwa kuwa ule ni mtandao wa kijamii sikuwa na haja ya kumjua sana, haikuwa na maana yoyote ile.
Picha za dokta Davis zilikuwa za kawaida sana na hakuonekana kama ni mtu anayeweza kuwa na msaada wowote. Ule udokta wake nikauchukulia kama ule wa kutafuta sifa facebook.

Haikupita siku bila Davis kunitumia ujumbe, sikumtilia maanani sana.
Siku moja majira ya jioni, nikiwa nimekaa chumbani kwangu, hasira zikiwa zinafukuta kichwani baada ya wanachuo wenzangu tuliokuwa tunaishi hostel moja jijini Mwanza, kunisimanga kuwa silipii umeme halafu ni bingwa wa kuutumia. Kwanza nilitaka kuulaani umasikini lakini nikahisi nitakuwa nauonea. Nikaanza kumlaani mwalimu Nchimbi, mume wake, baba na babu zao kwani niliamini kama wangefanya kazi kwa bidii bila shaka wangeupiga kikumbo umasikini.
Laana zangu, ambazo nilitaka kuzifikisha hadi kwa mizimu yao zilikatishwa na mlio katika simu yangu. Ulikuwa ujumbe umeingia. Niliogopa kuufungua maana niliamini ni watu wanaonidai. Nilitamani kuzima simu lakini nikakukumbuka kuwa nilikuwa nimem-bip mama yangu dakika saba zilizopita na alikuwa hajanipigia bado.

Nikapiga moyo konde nikaufungua ule ujumbe.
"Umepokea Tshs. 66,666 kutoka kwa Magreth Pearson. Salio lako jipya ni 66,666"
Zile laana zikakoma mara moja, mawazo yote yakahamia katika simu yangu. Nikausoma vyema tena ule ujumbe. Ulikuwa upo sahihi. Nilipoangalia salio langu kweli lilikuwa lieongezeka.
Nikajiuliza huyu Magreth ni nani. Jibu halikupatikana.
Nikazungusha kichwa huenda yupo mtu nilikuwa namdai jibu likawa hapana ni mimi nilikuwa nadaiwa.
"Huenda ni mtu kakosea kutuma!!!" likaja wazo hilo. Likachukua nafasi kubwa. Mara moja pepo la tamaa likaniingia nikamwomba msamaha kimoyomoyo huyo aliyetuma kimakosa. Kisha nikazima simu. Sikuwa nataka tena habari za mwalimu Nchimbi huko kijijini Makambako.
Upesi upesi nikakimbilia katika vibanda vya kutolea pesa nikawasha simu na kuitoa ile pesa upesi.
Kisha kwa mara nyingine nikazima simu tena.
Kitu cha kwanza niliwakata kidomodomo wanachuo walionisemasema. Nikalipia umeme!!!!
Heshima kidogo ikarudi!!! Usiku huo nilipika pilau, pilau yenye hadhi ya kuitwa pilau.
Najua iliwauma!!! Nilifanya makusudi!!!
Kesho yake baadhi wakawa marafiki zangu tena.
Baada ya siku tatu nikaiwasha simu yangu. Hapakuwa na meseji yoyote iliyoingia ikilalamika juu ya kukosea kutuma pesa!!!!
Sikuhangaika kujiuliza kulikoni.

*******

Ile pesa ilipokwisha nikarejea kwenye msoto kama ilivyo ada, nikawa najiliwaza katika mtandao wa kijamii wa facebook.
Kama kawaida Dokta Davis, alikuwa amesheheni katika kisanduku cha kuhifadhi ujumbe.
Leo Davis alikuwa na topiki nyingine kabisa, Dokta Davis alikuwa anazungumzia biashara ya mtandao.
Biashara ya mtandao?? Nikajiuliza…cha kushangaza kabla sijamuuliza hilo swali tayari alikuwa amenipa majibu.
Akaniuliza kama napenda kufanya biashara.
Kidogo nisimjibu maana kwa picha zake biashara kubwa kwake labda ya kuuza ubuyu karanga za kuchemsha. Sasa anataka kufanya biashara gani na mimi?? Nilijiuliza na kupatwa hasira kidogo. Lakini kwa kuwa sikuwa na kazi ya kufanya nikaendelea kuchat naye lakini vinginevyo nisingemjibu upuuzi wake aliotaka kuniambia.
"Unaweza kuvuna hadi milioni mbili…si lazima iwe mwisho wa mwezi!!!." Ujumbe wake ulisema. Mh!! Macho yakanitoka, nikaingiwa na dharau kabla ya kuendelea na mazungumzo hayo.
"Kivipi??" nilimuuliza ilimradi tu..
"Kirahisi sana." Alijibu. Sikuridhika na jibu lile nikambambika maswali mfululizo hatimaye Davis akanitumia kwa kirefu ni biashara gani hiyo aliyotaka kufanya nami na kwanini anichague mimi.
Baada ya dakika mbili nilikuwa nimemaliza kuusoma ujumbe mrefu wa Dokta Davis. Nilikuwa natetemeka, mapigo ya moyo yalikuwa katika mwendokasi wa kutisha sana. Macho yalikuwa hayafumbi bali yanaitazama simu yangu!!! Nilikuwa simuoni Dokta Davis lakini nilikuwa katika TAHARUKI!!!!!
SIKUAMINI!!!!!

*Ni kitu gani Isabella amekisoma hadi kumtisha hivyo…
**Je ni biashara gani hiyo ya mtandao.
*** Na kipi kilimsibu Isabellla baadaye!!!!

Thursday, February 9, 2017

Ray C_____Upepo (Cover)(Arithmeticmediagroup.blogspot.com)

Wema afikishwa Mahakamani na kusomewa mashtaka.


Sakata la Madawa: Wema Afikishwa Kortini Kisutu, Aachiwa Kwa Dhamana

Source;Global Publishers.                                   

Wema Sepetu na wafanya kazi wake wakipandishw akwenye karandiga la polisi kuelekea mahakamani.
DA RE SALAAM: Msanii wa Bongo Movie, Wema Sepetu na wafanya kazi wake wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na akusomewa mashtaka matatu ambayo yote yanahusiana na matumizi ya bangi.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Wema na wenzake hao wamekana mashtaka hayo na kuruhusiwa kupewa dhamana ya shilingi milioni 5 kila mmoja pamoja sambamba na kuwa na wadhamini wawili kila mtuhumiwa.

Kesi hiyo inaendeshwa na Hakimu wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba ambapo mawaakili kwa upande wa watuhumiwa ni Alberto Msando na upande wa serikali ni Pamela Shinyambara pamoja na Nassoro Katuga.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 28 mwaka huu itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Wema na wenzake wakishuka mahakamani Kisutu

Kamanda wa Polisi wa Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro jana alesema kuwa jeshi lake bado linamshikilia Wema na wenzake saba ambao walikamatwa na vielelezo na kuwa jalada lao limepelekwa kwa wakili wa serikali alipitie ili aone ushahidi uliopo pamoja na kupata majibu kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kubaini kama kweli ni mtuamiji wa madawa ya kulevya na baada ya hapo atafikishwa mahakamani.

Wednesday, February 8, 2017

New Audio;Rummy ft Linah_____Mwari(Arithmeticmediagroup.blogspot.com)

New Audio;Sadimu Mavoice_____Minduna(Arithmeticmediagroup.blogspot.com)


New Audio;Samir_____I Will Marry You(Arithmeticmediagroup.blogspot.com)


New Audio;Sticko Ft. Yamoto Band_____Linah(Arithmeticmediagroup.blogspot.com)


New Audio;Stone ft Belle 9_____Nahisi(Arithmeticmediagroup.blogspot.com)



New Audio;Sultan King_____Sitaki Lawama(Arithmeticmediagroup.blogspot.com)



Mfahamu shetani ni nani na Historia yake.

 

Shetani ni Nani?

THOMAS S KAFUMU-IGUNGA-TABORA.

Hivi shetani ni nani? Biblia humwita “Mungu wa ulimwengu huu.” Lakini alitoka wapi? Je Mungu alimuumba kama alivyo? Je, yeye ni roho aliyeanguka? Haya hapa ni majibu kutoka katika Neno la Mungu!

Shetani amekuwa somo lenye shauku kubwa kwa maelfu ya miaka. Amedhaniwa kuwa kama jini, mzuka, na zimwi. Ama kama mtu mwenye sura nzuri ya “kishetani” aliyevalia suti nyekundu, mwenye pembe na uma ya nyasi. Shetani hata amesimuliwa kuwa kama kitu kisicho dhahiri “aliye muhtasari wa maovu yote.” Au kama chanzo cha kila kitu kibaya watendacho watu. Huenda wengi wanaufahamu usemi “shetani alinifanya nitende.” Ingawa fikira hizi ni za kawaida, zote SI SAHIHI! Hata zinapojumuishwa pamoja, kwa kiwango kikubwa zinamwakilisha isivyo roho huyu mkuu aliyeanguka!
Wengi wanaojiita Wakristo hutoa risala ndefu, kwa sauti kubwa juu ya “yule mwovu mbaya wa zamani.” Makundi mengi yenye misisimko huendesha mikutano kwenye mahema, kampeni, mikesha na harakati za kidini mahali ambapo watu huambiwa, “Tunakwenda kumwangusha chini yule mwovu usiku wa leo.” Idadi kubwa ya watu huondoka katika mikutano hii wakiwa wameshawishika kabisa kwamba wamefanya hili.
Hawako sahihi! Hawajafanikisha chochote zaidi ya hisia za kitambo za kujiridhisha wenyewe. Kwa bahati mbaya, shetani pia huondoka katika mikutano hii akijisikia hata kutosheka zaidi kutokana na kile alichokishuhudia—na kukisababisha!
Ni wachache wanaoujua UKWELI juu ya shetani ni nani na ni nini. Kijitabu hiki kitafutilia mbali fumbo, mkanganyiko, ujinga, kisasili (hadithi za kubuni), ushirikina na nadharia zisizosahihi zinazogubika ukweli juu ya utambulisho na asili yake.

Kuvutiwa na Shetani Kunakoongezeka

Mara chache sana mtu atazunguka huku na huku pasipo kusikia na kuona vidokezo juu ya shetani au mapepo. Tulia kwa muda na ufikiri juu ya mara ngapi hili hutokea.
Fungulia runinga. Nenda kwenye nyumba za sinema. Tembelea duka la vitabu. Ni mara ngapi somo la shetani, mapepo, malaika au ulimwengu wa roho huongelewa au kuandikwa kwa jumla? Mifululizo mizima ya vipindi vya runinga hutengwa mahsusi kwa ajili ya masomo haya, na vingine zaidi vikitokea kila wakati. Kwa miaka mingi sinema zimemlenga (zimemfokasi) shetani. Lakini sasa zinakuja mara nyingi zaidi—na ni za ajabu zaidi, zenye vioja, ngeni, za kutisha na kutia hofu kuliko hapo awali!
Fikiria shani ya “Harry Potter.” Baadhi ya waandishi karibu kabisa hawaandiki juu ya kitu kingine zaidi ya ulimwengu wa roho, mara nyingi wakichanganya ufahamu wa uongo wa unabii katika njama yao—na majeshi ya mashabiki hununua kila moja ya vitabu vyao.
Ushetani na uchawi vinatekelezwa kwa wazi zaidi kuliko hapo kabla!
Mamilioni hutumia kiasi kikubwa cha fedha kupiga simu za moja kwa moja kwa watabiri, wasoma viganja, wanajimu, watazama bao, wasihiri, wapiga ramri na kundi lingine la wenye kuwasiliana na mizimu, kutaka kujua nini kitawatokea siku za usoni.
Shetani huuza—na watu wananunua zaidi kuliko hapo kabla!

Mkanganyiko Usio wa Lazima

Mtume Paulo aliandika, “Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani; vile vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu” (1 Kor. 14:33). Wakati MKANGANYIKO mkubwa umegubika utambulisho wa shetani, huhitaji kukanganyikiwa!
Biblia ndiyo msingi wa maarifa yote. Mara kwa mara utatusikia tukisema, “Futa vumbi lililofunika Biblia yako! Ichunguze kwa makini na uone ukweli halisi ambao umekuwepo wakati wote katika kurasa zake. Usiamini chochote kwa sababu tu tumekisema, bali kiamini tu ikiwa umekiona kimethibitishwa ndani ya Biblia yako.”
Biblia inabeba majibu ya maswali yote makubwa ya maisha! UKWELI DHAHIRI wa maagizo yake haufundishwi katika makanisa ya ulimwengu huu. Tangu mapema kama “Shule ya Jumapili,” wengi wanafundishwa kuamini kile ambacho kila mmoja hudhania kimo ndani ya Neno la Mungu. Kile ambacho Biblia husema kuhusu asili ya mwovu Shetani kitakushangaza. Lazima tuiache Biblia imfunue jinsi alivyo.
Paulo pia aliandika, “JARIBUNI mambo yote; lishikeni lililo jema” (1 The. 5:21), na “MPATE KUJUA hakika mapenzi ya Mungu, yaliyo mema, yakumpendeza, na ukamilifu” (Rum. 12:2).
Tutayachunguza mafungu yanayofafanua asili ya shetani na kwamba yeye ni nani. Ili kufanya hivi, ni lazima tuachane na fikira za kibinadamu na tukubali tu kile kinachoweza kuthibitishwa ndani ya Biblia!

Shetani Alitoka Wapi?

Shetani yuko hai na halisi. Biblia inamuita “mungu wa ulimwengu huu” (2 Kor. 4:4). Ufunuo 12:9 husema kwamba “audanganyaye ulimwengu wote.” Kwa hakika hii hujumuisha ukweli juu ya utambulisho wake. Lakini je wakati wote amekuwa shetani? Wakati wote amekuwa yule mwovu, muuaji, mwongo, mkuu wa giza mharabu? Je aliumbwa jinsi hiyo?
Hakuwa hivyo!
Maswali haya yanahitaji ufafanuzi. Yale ambayo utayasoma yatakusaidia uione picha kamili. Biblia humwelezea shetani katika maandiko mengi. Kijitabu hiki kimsingi kinachunguza mafungu yanayofafanua asili ya shetani. (Kijitabu chetu kikubwa, Ulimwengu Matekani, hujadili maandiko mengi yanayoelezea jukumu, mkakati na hila zake. Soma kijitabu hiki cha rejea upate kuelewa kwa ujumla namna shetani anavyotenda kazi.)
Mwanzoni Mungu aliumba makerubi watatu: Lusifa au Nyota ya Alfajiri (aliyegeuka kuwa Shetani), Mikaeli na Gabrieli. Kila mmoja alitawala theluthi ya mamia ya mamilioni ya malaika (Ufu. 5:11). Nyota ya Alfajiri na theluthi yake walitawala ulimwengu uliokuwa kabla ya Adamu. Yeye, pamoja na malaika zake, waliasi serikali ya Mungu, na leo anawaongoza malaika hawa walioanguka, au mapepo, kama mungu wa dunia hii.

Mwanzo 1

Mwanzo 1:1 inasema, “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi.” Andiko hili linaweka jukwaa kwa ajili ya somo letu.
Kitabu cha Ayubu kinaeleza vyema wakati ambapo Mungu aliiumba dunia, miaka mabilioni iliyopita. Mungu alimuuliza Ayubu mfululizo wa maswali: “Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya nchi? Haya! Sema, kama ukiwa na ufahamu. Ni nani aliyeamrisha vipimo vyake, kama ukijua? Au ni nani aliyenyosha kamba juu yake?…Hapo nyota za asubuhi zilipoimba pamoja, Na wana wote wa Mungu walipopiga kelele kwa furaha?” (38:4-5, 7).
‘Nyota” hizi walikuwa malaika (Ufu. 12:4), pia wameelezewa kama “wana wa Mungu.” (Bila shaka, nyota halisi haziimbi.) Angalia kwamba inasema “wote” “walipaza sauti” na “kuimba pamoja.” Palikuwa hapajawa na mapepo wabaya bado wakati wa uumbaji katika Mwanzo 1:1.
Andiko hili linaonyesha kwamba nchi iliumbwa katika hali ya ajabu na maridadi. Kulikuwa na furaha tele na uimbaji. Sasa soma Mwanzo 1:2.
Fungu hili limetafsiriwa isivyo na haliakisi maana ya Kiebrania asili. Biblia ya King James Version inasema, “Nayo nchi ilikuwa ukiwa tena utupu.” Maneno matatu muhimu ya Kiebrania yametafsiriwa isivyo hapa, hivyo kuzuia, na kwa hakika kuficha, maana halisi ya fungu isionekane.
Neno lililotafsiriwa “ilikuwa” ni hayah. Katika Mwanzo 2:7, neno hili limetafsiriwa kwa usahihi “a’kawa,” na katika Mwanzo 9:15, “hayata’kuwa.”
Maneno kwa ajili ya “ilikuwa ukiwa, tena utupu” ni tohu na bohu. Yakitafsiriwa kwa usahihi, yanamaanisha “vurumai, katika mkanganyiko, ukiwa na utupu.” Kwa ufupi, nchi iliyoumbwa kamilifu (fu. 1), “ikawa vurumai na iliyokanganyikiwa” (fu. 2). Tohu na bohu yametafsiriwa kiusahihi katika Yeremia 4:23. Isaya 34:11, miongoni mwa sehemu zingine, inatafsiri usemi huu kama “mkanganyiko na utupu.”
Angalia Isaya 45:18, inayobainisha namna ambavyo Mungu hakuiumba dunia: “Maana BWANA, aliyeziumba mbingu asema hivi, Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa [tohu kumaanisha vurumai au utupu], aliiumba ili ikaliwe na watu.” Ni wazi kwamba dunia ilikuja kuwa vurumai baada ya Mungu kuiumba—katikati ya matukio yaliyoelezewa katika Mwanzo 1:1 na 1:2. Fungu la mwisho linaelezea KU-umbwa upya kwa dunia miaka 6,000 iliyopita, na fungu la 1 linaelezea uumbaji wa kwanza wa ulimwengu mzima ambao, kulingana na wanasayansi, ulifanyika kadiri ya miaka bilioni 17 iliyopita.
Zaburi 104:30 inasema kwamba Mungu “aufanya upya uso wa nchi.” Zile siku saba za juma la uumbaji ni wakati ambapo Mungu aliikarabati upya dunia iliyoharibiwa, iliyoumizwa, iliyokuwa kwa wakati huo imefunikwa kabisa na maji (Mwa. 1:2). Tutakuja kuona kwamba hii ilisababishwa na shetani. Matendo 3:19-21 hufunua kwamba ni Kurudi kwa Kristo tu ndiko kutakakoleta “urejeshaji [kurejesha] wa vitu vyote.”
Sasa tunajua kile kilichotokea. Lakini kilitokea kwa namna gani? Ni kwa namna gani dunia ilibadilika kutoka kuwa maridadi na kamilifu wakati wa kuumbwa hadi kuwa vurumai, iliyokanganyikiwa, ukiwa na utupu? Kwa kuwa Mungu si Mungu wa machafuko (1 Kor. 14:33), tunajua kwamba Hakuiharibu dunia. Basi ni nani au ni nini kilisababisha hili?

Isaya 14

Biblia hufunua ukweli muhimu juu ya somo lolote ikiwa mtu atasoma maandiko yote yanayohusika nalo. Tukiwa na hili kichwani, hebu tusome juu ya Nyota ya Alfajiri baada ya kuwa Shetani.
Isaya 14:12-15 inaelezea hadithi isiyo kifani iliyo na viashiria kuhusu mahali ambapo Nyota ya Alfajiri alishawahi kuwa, alichofanya na kilichomtokea. Soma kwa makini, ukizingatia semi maalumu zilizotiliwa mkazo: “Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu: Nitafanana na yeye Aliye juu. Lakini utashushwa mpaka kuzimu [“kaburini”—mafungu ya 9 na 11], Mpaka pande za mwisho za shimo.”
Yule aliyeitwa “Nyota ya alfajiri” isingewezekana kwamba alikuwa mtu. Mambo aliyoyafanya hayawezi kutendwa na mwanadamu awaye yote. Ni shetani pekee “huyaangusha mataifa” na kwamba alisema “angepanda mpaka mbinguni.” Kwa hakika hakuna mtu ambaye angeweza “kushushwa mpaka kuzimu” kwa jinsi ilivyoelezewa hapa. Mwisho, hakuna mtu aliye na kiti cha enzi ambacho kingeweza kuwekwa juu kuliko “nyota za mbinguni.”
MUNGU huishi katika upande wa kaskazini wa mbingu au “pande za kaskazini.” Ayubu anaangazia jaribio la Nyota ya alfajiri la kutaka kumpindua Mungu mahali pale: “Yeye [Mungu] hutandaza kaskazi juu ya nafasi isiyo na kitu, Na kuutundika ulimwengu pasipo kitu” (26:7). “Nafasi isiyo na kitu” ya “kaskazini” huafikiana na kile ambacho wanajimu wamekiona kuwa ni sehemu isiyo ya kawaida yenye upungufu wa nyota katika mwelekeo huo. Bila shaka, Shetani alimvamia Mungu katika mwelekeo huo wakati alipotafuta kujiinua kutoka kwenye kiti chake cha enzi ili kukikalia kiti cha enzi cha Mungu katika “pande za kaskazini.” Hiki ndicho Biblia inachokifunua!

Ezekieli 28

Ezekieli 28:12-17 huenda sambamba na hutilia mkazo Isaya 14, na ni muhimu nayo tukaisoma. Kifungu hiki kinaelezea kile ambacho baadhi ya “wasomi” hudai alikuwa mwanadamu “mfame wa Tiro.” Usomaji wa makini huonyesha hiki hakiwezekani—na ni upuzi.
Fungu hili huongelea juu ya mmoja ambaye “hutia muhuri kipimo, umejaa hekima, na ukamilifu wa uzuri,” ambaye pia “alikuwa ndani ya Edeni, bustani ya Mungu.” Hakuna mwanadamu aliyewahi kuwa mkamilifu, huyu alikuwa ni shetani—joka—aliyemdanganya Hawa pale Bustanini. Fungu la 13 husema, “katika siku ya kuumbwa kwako,” na Shetani ni kiumbe aliyeumbwa. Fungu la 14 humwita “kerubi afunikaye.” (Kutoka 25:17-20 huelezea “makerubi wawili waaminifu waliobaki wa[lio]funika” kiti cha enzi cha Mungu katika hema ya Agano la Kale. Mabawa yao hufunika “kiti cha rehema.”) Maelezo haya hayawezi kuwa ya mfalme yeyote wa kidunia.
Sehemu ya mwisho ya Ezekieli 28:14 inasema kwamba “mfalme” huyu alikuwa “katika mlima wa Mungu” na “alitembea…kati ya mawe ya moto.” Hii huelezea eneo linalozunguka kiti cha enzi cha Mungu. Fungu la 15 hutamka, “uovu [uvunjaji wa sheria] ulipoonekana ndani yako” na fungu la 16 linaurejelea kama “dhambi.”
Fungu la 16 pia humwelezea kerubi huyu kama aliyekuwa “ametolewa…nje ya” mbingu. Mungu pia alisema “angemwangamiza” (Kiebrania: fukuzia mbali) Nyota ya alfajiri kutoka mbinguni. Fungu la 17 hufunua kwamba “moyo wake uliinuka kwa sababu ya uzuri [wake]” na kwamba “hekima yake iliharibiwa… kwa sababu ya mwangaza [wake].” Fungu hili linamalizikia kwa Mungu “kumtupa chini,” mahali ambapo wafalme wa dunia wangepata “”kumtazama.”
Nyota ya alfajiri alikuwa ni kiumbe mwenye akili sana—“malaika wa nuru,” kama walivyo “watumishi wake” (2 Kor. 11:13-15). Jina Nyota ya alfajiri lina maana ya “mwenye kuleta nuru.” Kiumbe huyu aliyekuwa mkamilifu hapo awali alileta nuru ing’arayo kwa wote waliokuwa wakimzunguka. Lakini aliasi na kutenda dhambi—na hivyo kuwa “mkuu wa giza.” Uasi wake ukamgeuza kuwa kiumbe aliyepinda, aliyepotoka. Japokuwa ni mwenye akili nyingi, kwa hakika amekuwa malaika kichaa aliyeanguka, asiyejua kutofautisha jema na baya!

Mnyama na Nabii wa Uongo

Ufahamu wa ziada kuhusu unabii fulani nyeti, ambao haujatimia ni wa lazima kabla ya kuendelea na kile kilichomtokea Shetani alipotupwa duniani.
Watu wawili, wanaojulikana kama “mnyama na nabii wa uongo,” watauongoza mfumo wa mwisho wa kidini-na-kiselikali wenye nguvu ulioonyeshwa kwenye Ufunuo 17 na 18, ambao Kristo ataupondaponda na kuchukua mahala pake katika Kurudi Kwake. Ufunuo 16:13-14 huelezea roho za mashetani kama zikiwa na nguvu ya “kufanya miujiza” kupitia mfumo huu. Mnyama akiwa ndiye kiungo kikuu cha mfumo huu, atakuwa mtu mkuu atawalaye ulimwengu.
Nabii wa uongo naye, ataongoza ulimwengu kumwabudu mnyama kama Mungu (Ufu. 16:2; 19:20)! Udanganyifu huu utaenea sana (18:3)—kwa ukamilifu—kiasi kwamba watawadanganya wanadamu wote kufikia kupigana na Kristo katika Kuja Kwake Mara ya Pili (16:9, 13-16; 17:13-14)!
Sasa angalia 2 Wathesalonike 2:3-4 na 8. Fungu la 3 humrejelea yule anayeitwa “mtu wa kuasi” na “mwana wa uharibifu; yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.” Nabii wa uongo naye pia hudai kwamba ni Mungu.
Linganisha hiki na Ezekieli 28:2 na kielelezo cha “mfalme wa Tiro”—mwanadamu. Ezekieli aliandika kwamba “mfalme” huyu husema “Mimi ni Mungu, naketi katika kiti cha Mungu,” 2 Wathesalonike 2:8 humwelezea huyu “mtu wa kuasi” kama “[yule] mwovu” ambaye “atafunuliwa” namna vile alivyo wakati Kristo anaporudi na kumwangamiza pamoja na mnyama katika ziwa la moto (Ufu. 19:20). Isaya 14:4 humrejelea nabii wa uongo kama “Mfalme wa Babeli.” Huyu ndiye yule yule “Mfalme wa Tiro,”
Ukiendelea katika 2 Wathesalonike 2, fungu la 9 hutoa kauli ya kushangaza juu ya nabii wa uongo. Inasema kwamba “kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo.” Fungu la kumi huonyesha kwamba anaweza kumdanganya kila mmoja “asiyependa kweli.” Fungu la 11 hufunua kwamba Mungu ataleta “nguvu ya upotevu” kwa wote ambao kwa utashi wao huamini uongo wake.
Viongozi wa mfumo huu mkuu wa uongo watakuwa wamepagawa moja kwa moja na shetani! Hali hii itampatia nabii wa uongo nguvu nyingi sana za kudanganya na kutenda miujiza. Shetani, ambaye wakati wote ametamani kumpindua Mungu na kuchukua mahali pake, atanena kupitia mtu huyu ambaye ni kiongozi wa kidini na kuutangazia ulimwengu wote kwamba, hakika yeye ni, MUNGU! Onyo hili la Biblia halina utata. Miujiza atakayotenda itawadanganya walio wengi sana miongoni mwa watu!
Je, utadanganywa wakati matukio haya yatakapoanza kutokea hivi karibuni—maana hakika yatatokea? (Soma kijitabu chetu Nani au ni Nini Mnyama wa Ufunuo? Kujifunza zaidi juu ya huyu kiongozi wa mwisho wa ulimwengu.)

Alitupwa Hata Nchi na Malaika Zake Wote

Ufunuo 12 husema juu ya Shetani na pepo wake wabaya “walitupwa katika nchi” (fu. 13). Kwa hakika sura hii imepachikwa katikati ya kitabu cha Ufunuo, na ni muhtasari mfupi wa historia ya Kanisa la Agano Jipya.
Fungu la 3 linamwelezea Shetani kama “joka” aliye “kokota theluthi ya nyota za mbinguni na kuziangusha katika nchi” (fu. 4). Kumbuka kwamba “nyota” hizi zilikuwa ni theluthi ya malaika wote waliokuwa chini ya Nyota ya alfajiri kabla hajaasi.
2 Petro 2:4 hutoa kiashiria kingine juu ya huku “kutupwa chini” kwa Shetani na malaika zake “aliowakokota pamoja” naye. Angalia: “Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa [Shetani hakuwa malaika pekee aliyeasi], bali aliwatupa shimoni.” (Neno la Kigiriki hapa ni tartaros na linamaanisha aidha “gerezani” ama “kizuizini”—hii ni dunia yenyewe.) Pepo hawa wabaya pamoja na Shetani “wanalindwa hata ije hukumu,” wakiisha “kutiwa…katika vifungo vya giza.” Hii inafunua kwamba Mungu aliwatia katika gereza hili la giza pepo wengine wengi walioanguka waungane na “mkuu wa giza.”
Ufunuo 12:7-9 hueleza, kwa undani, lini Shetani na pepo wake wabaya watatupwa hata nchi kwa mara ya mwisho wasipate tena kibali cha kuingia mbinguni. Mafungu ya 12-14 yanaonyesha kwamba mwitikio wa ibilisi ni hasira kuu. Wakati huu wa kutisha unakuja kwa ulimwengu mzima hapo mbeleni kidogo!

Hatima ya Shetani

Lakini kitatokea nini kwa Shetani mara baada ya Kurudi kwa Kristo? Je, ataachwa huru kurandaranda duniani, akiendelea “kudanganya” (Ufu. 12:9) na “kudhoofisha” (Isa. 14:12) mataifa? Je, ataruhusiwa kubakia kuwa “mungu wa ulimwengu huu” (2 Kor. 4:4) milele? Hatima yake ni nini?
Ufunuo 20 huelezea Kristo akisimamisha utawala wa milenia kwa miaka-1000 (fu. 4) na kuzileta “sura za mwisho” katika kisa cha Shetani. Fungu la 2 husema kwamba malaika mwenye nguvu (fu. 1) anamfunga hakika kwa “miaka elfu” na “kumtupa katika kuzimu,” mahali “anapofungwa.” Kisha malaika huyu “[hu]tia muhuri juu yake, kwamba asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie: na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache.”
Paulo alitaja wakati wa Shetani kufungwa aliposema, “naye Mungu wa amani atamseta Shetani chini ya miguu yenu upesi” (Rum. 16:20). Hii ni ahadi ya Mungu kwa Wakristo wote wa kweli na wanadamu wote, kwa sababu Shetani amewatesa Wakristo na kawadanganya wanadamu kwa maelfu ya miaka!
Mtume Yuda alisema kwamba Shetani na pepo wake wabaya watatupwa nje ya mifumo ya sayari kwenda mahali ambapo Biblia hupafafanua kuwa hapana nuru. Fungu la 13 huwaongelea viumbe hawa wenye kudhalilika kama “nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba yao waliyowekewa milele.” Yule “mkuu wa giza” na malaika zake watapata kile wanachostahili—kile walichojiletea wao wenyewe. Yule ambaye hapo awali alijulikana kama “aletaye nuru” alichagua giza. Mungu atampatia giza kamili kwa muda wote utakaofuata!

Uwezekano Wako Mkuu

Waebrania 2:5 huelezea dunia chini ya “utawala wa malaika [halisi]” sasa, lakini inaweka wazi kwamba malaika hawa hawataendelea kuutawala “ulimwengu ujao.”
Mafungu ya ziada katika sura hii hufafanua kile kitakachotokea wakati malaika walioanguka wanaotawala ulimwengu huu sasa watakapoondolewa na mahali pao kuchukuliwa: “Mwanadamu ni nini hata umkumbuke?…Umemfanya mdogo punde kuliko [maelezo ya ziada: chini ya] malaika, Umemvika taji ya utukufu na heshima… Umeweka vitu vyote chini ya nyayo zake. Kwa maana katika kuweka vitu vyote chini yake hakusaza kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hatujaona vitu vyote kutiwa chini yake” (fu. 6-8).
Yakiongelea juu ya Kristo, mafungu ya 9-10 huendelea, “ila twamwona yeye aliyefanywa mdogo punde kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji ya utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu. Kwa kuwa ilimpasa…akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso.”
Je, ulishika—kamata—kile kilichosemwa? Mafungu haya yamebeba ahadi ya uwezekano wa kuduwaza unaopatikana kwako na kwangu. Wakristo wameitwa kurithi “vitu vyote” na wapate “kuvikwa taji ya utukufu na heshima,” vilivyoahidiwa kwao kutokana na mwito wa Mungu na dhabihu ya Kristo—kiongozi mkuu wa wokovu wao.”
Hakuna utata kuhusu nini maana ya “vitu vyote”. “Hakuna kitu” (fu. 8) kitakachowekwa kando katika urithi huu. (Soma vijitabu vyetu vya bure Nini Thawabu Yako Katika Maisha Yajayo?, Ufalme wa Mungu ni Nini? na Hivi Wokovu ni Nini?, miongoni mwa vingine, kujifunza zaidi juu ya uwezekano wa kushangaza unaowangojea watakatifu wote wa kweli wa Mungu.
Katika Mathayo 4:9, Shetani alimwahidi Kristo utawala juu ya “vitu vyote” kama “angeanguka chini na kumsujudia.” Wakristo wameahidiwa utawala juu ya “vitu vyote” hivyo hivyo—lakini kwa sharti pekee kwamba wamwabudu Mungu wa kweli!

Shetani Afunuliwa

Herbert W. Armstrong alihitimisha kijitabu chake Je, Mungu Aliumba Shetani? na:
“Mungu alimweka kerubi mkuu, Nyota ya alfajiri, kusimamia serikali Yake duniani, lakini Nyota ya alfajiri alikataa kutekeleza mapenzi ya Mungu, amri za Mungu, serikali ya Mungu. Alitaka kuibadili na ya kwake mwenyewe. Hivyo akajiondolea sifa yeye mwenyewe.
“Adamu alikuwa na nafasi ya kutwaa mahali pake. Katika kinyanganyiro cha kuona kama Adamu angeshinda, kama angemtii Mungu, alishindwa. Badala yake alimtii ibilisi, na mwanadamu akawa mali ya ibilisi, na tangu hapo jamii yote ya binadamu ikawa imeuzwa kutelemkia mtoni kwa ibilisi.
“Yesu Kristo akaja miaka 4,000 baadaye na akaingia katika shindano hilo kubwa—shindano la kujaribiwa pale Mlimani. ALIKATAA kumtii ibilisi. Alinukuu maandiko kwa usahihi. Alimtii Mungu.
“Hatimaye, Alimgeukia ibilisi, na akampa Shetani amri. Alisema ‘Nenda zako Shetani,’ na ibilisi akatii!
Kutoka wakati huo na kuendelea, mrithi wa Shetani alifuzu kuchukua utawala wa dunia. Lakini Yesu alienda mbinguni kwa miaka 1,900. Atarudi tena hivi karibuni, na atakaporudi, ibilisi ATAONDOLEWA KUTOKA MAHALI PAKE. Kristo ataitawala dunia, Amri za Mungu zitarejeshwa. Hatimaye mpango sahihi na amani vitakuja!
“Kwa hiyo Mungu HAKUUMBA ibilisi. Aliumba kerubi, Nyota ya alfajiri—mkamilifu katika njia zake, lakini akiwa na nguvu ya uchaguzi huru—na Nyota ya alfajiri alijigeuza mwenyewe akawa shetani kwa kuasi Serikali ya Mungu!’

Monday, February 6, 2017

Addicted_____Eddy Kenzo ft. Alaine(Arithmeticmediagroup.blogspot.com)


AY Ft. Nyashinski_____More and More(Arithmeticmediagroup.blogspot.com)


Braytone_____Nitampata(Arithmeticmediagroup.blogspot.com)


B-Red_____Fall For You(Arithmeticmediagroup.blogspot.com)


Brown Mauzo_____Sitaki Apotee(Arithmeticmediagroup.blogspot.com)


Cjamoker Ft. Wakazi & Country Boy_____ Bongo Most Wanted(Arithmeticmediagroup.blogspot.com)


Country Boy_____Macho Mbele(Arithmeticmediagroup.blogspot.com)


Dully Sykes_____Yono(Arithmeticmediagroup.blogspot.com)


Godzilla ft G Nako_____Kila Wakati(Arithmeticmediagroup.blogspot.com)